Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) Novemba, 2020
Katibu Mtendaji, Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) anapenda kuwajulisha watu wote wanaotarajia kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) Novemba, 2020 kama Watahiniwa wa Kujitegemea kwamba;
- Kipindi cha usajili kwa Watahiniwa wa Kujitegemea kitaanza tarehe 01/01/2020 kwa ada ya Shilingi 50,000/= kwa wanaojisajili CSEE na Shilingi 30,000/= kwa wanaojisajili QT na kitaishia tarehe 29/02/2020. Aidha, watakaojisajili kwa kuchelewa kuanzia tarehe 01/03/2020 hadi tarehe 31/03/2020 watalipa Shilingi 65,000/= kwa Watahiniwa wa Kidato cha Nne (CSEE) na Shilingi 40,000/= kwa Watahiniwa wa Mtihani wa Maarifa (QT) ikiwa ni ada ya kawaida pamoja na faini.
- Mtahiniwa atakaye jisajili kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) 2020 ni yule ambaye anarudia Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) au amefanya na kufaulu Mtihani wa Maarifa (QT) katika kipindi kisichozidi miaka mitano (5) iliyopita au mwenye sifa zinazolingana na hizo alizopata kutoka nje ya Nchi na kufanyiwa ulinganifu na Baraza la Mitihani la Tanzania.
- Mtahiniwa atakaye jisajili kufanya Mtihani wa Maarifa ni yule ambaye anatafuta sifa ya kufanya Mtihani wa Kidato cha Nne kama Mtahiniwa wa kujitegemea.
- Usajili unafanyika kwa njia ya mtandao, kwa kufuata utaratibu ufuatao;
- Fika Kituo utakachofanyia Mtihani ili kupata namba rejea (Reference Number) ambayo inatolewa bure.
- Fika Ofisi ya Posta kupata ‘Control Number’ ya kufanyia malipo ya ada ya Mtihani au ingia katika tovuti ya Baraza la Mitihani ili utengeneze ‘Control number’ ya kufanyia malipo kwa utaratibu ulioelekezwa.
- Fanya malipo ya ada ya Mtihani kupitia Posta au Benki kwa kutumia ‘Control Number’.
- Fika Posta kufanya usajili au jisajili mwenyewe kupitia tovuti ya Baraza la Mitihani.
- Baada ya usajili kukamilika wasilisha nakala moja ya fomu Ofisi ya Posta, wasilisha nakala ya pili kwenye Kituo utakachofanyia Mtihani na nakala ya tatu ya fomu itunzwe na wewe (mtahiniwa) mwenyewe kwa ajili ya kumbukumbu.
Source:- necta